IQNA

OIC yaahidi kuwasaidia Waislamu wa Rohingya, yakiri kuzembea

11:31 - May 06, 2018
Habari ID: 3471497
TEHRAN (IQNA)-Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Kiislamu (OIC) imeahidi kuchukua hatua imara kutatua kadhia ya Waislamu wa jamii ya Rohingya wanaokandamizwa nchini Myanmar huku wengi wao wakikimbilia Bangladesh kuokoa maisha yao.

“Tutashirikiana na Bangladesh, Umoja wa Mataifa na jamii ya kimataifa kuwasaidia Waislamu Warohingya,” amesema Hesham Youssef, Naibu Katibu Mkuu wa OIC anayeshughulikia masuala ya kibinadamu baada ya kutembelea kambi za wakimbizi Warohingya eneo la Kutupalong nchini Bangladesh.

Ameongeza kuwa utawala wa Myanmar unapaswa kuendelea kushinikizwa ili kuwaruhusu Waislamu Warohingya kurejea katika ardhi zao za jadi.

Youssefi aidha amekiri kuwa nchi za Kiislamu zimezemba na kubainisha masikitiko yake kuwa OIC haikuchukua hatua za haraka kuwasaidia Waislamu Warohingya wakati wimbi jipya la mashambulizi dhidi ya jamii hiyo lilipoanza Agosti mwaka jana katika jimbo la Rakhine nchini Myanmar. Tokea wakati huo Waislamu zaidi ya laki saba wamekimbilia nchi jirani ya Bangladesh kufuatia maangamizi ya kimbari ambayo yamekuwa yakitekeleza dhidi yao na jeshi la Myanmar.

Jinai kubwa wanazofanyiwa Waislamu hao na wanajeshi na Mabudha wa nchi hiyo  wenye misimamo ya kufurutu katika mkoa wa Rakhine magharibi mwa Myanmar zilishika kasi tangu tarehe 25 mwezi Agosti mwaka 2017. Hadii sasa  jina hizo zimepelekea kuuliwa Waislamu zaidi ya elfu sita na kujeruhiwa maelfu ya wengine huku wengine zaidi ya laki saba wakilazimika kuwa wakimbizi katika nchi jirani za Bangladesh na India.

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa uhalifu unaofanywa na Mabudha kwa himaya ya jeshi la Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya ni mauaji ya kimbari.

Zeid Ra'ad Al Hussein anasisitiza kwamba, kuna udharura wa kufika katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo na kufanya uchunguzi kuhusu ukatili unaofanywa na serikali ya Myanmar dhidi ya Waislamu.

3465723

captcha