IQNA

Rais wa Afghanistan atangaza usitishwaji mapigano na Taliban wakati wa Idul Adha

0:50 - August 20, 2018
Habari ID: 3471637
TEHRAN (IQNA)- Rais Mohammad Ashraf Ghani wa Afghanistan ametangaza usitishwaji vita wenye masharti na kundi la wanamgambo wa Taliban kabla ya SIku Kuu ya Idul Adha kuanzia Jumatatu.

Akizungumza Jumapili, rais Ghani amesema muafaka huo wa usitishaji mapigano utaendelea hadi Maulid ya Mtume Muhammad SAW ambayo itaadhimishwa kitaifa nchini Afghanistan Novemba 21. Amesema sharti kuu la muafaka huo ni kuwa kundi la Taliban nalo lisitishe mapigano.

Rais Ghani akuhutubu  wakati wa sherehe za kuadhimisha mwaka wa 99 wa uhuru wa Afghanistan mjini Kabul, ameongeza kuwa uamuzi huo umefikiwa baada ya mashauriano na wadau mbali mbali katika jamii ya Afghanistan na wanazuoni wa Kiislamu kote duniani.

Tangazo la Rais Ghani limehusi Taliban tu na halikuhusisha makundi mengine hasa kundi la kigaidi la ISIS au Daesh.

Kundi la Taliban hadi sasa halijatoa kauli yoyote kuhusiana na suala la usitishaji vita wa pamoja na serikali ya Kabul lakini limesema litaachilia huru ‘mamia ya wafungwa’ kwa munasaba wa Idul Adha. Ikumbukwe kuwa tarehe 12 Juni mwaka huu yaani katika siku ya Iddil-Fitri, serikali ya Afghanistan ilitangaza usitishaji vita wa wiki moja na kundi la Taleban, ingawa kundi hilo lilikubali usitishaji vita wa siku tatu pekee.

3739898

captcha