IQNA

Yemen yalaani hatua ya Saudia kuwazuia Waislamu kuhiji

23:20 - June 13, 2021
Habari ID: 3474002
TEHRAN (IQNA)- Wizara ya Hija ya Yemen imelaani vikali hatua ya Saudia kuwazuia Waislamu kutoka nje ya ufalme huo kutekeleza ibada ya Hija.

Taarifa ya wizara hiyo imesema kitendo cha Saudia kuwazuia Waislamu kutekeleza ibada ya Hija kwa mwaka wa pili mfululizo si sahihi.

Wizara ya Hija ya Yemen imesema utawala wa Saudia unapaswa kuruhusu ibada ya Hija kwa sharti la uzingatiwaji kanuni za kiafya. Aidha taarifa hiyo imesema wanaofaidika na kitendo hicho cha Saudia ni maadui wa Uislamu wakiongozwa na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel kwani kwa mtazamo wao Hija ni sawa na kongamano la Kimataifa la Kiislamu ambalo huimarisha umoja wa Waislamu.

Wizara ya Hija ya Yemen imetoa wito kwa Waislamu duniani kulaani kitendo hicho cha Saudia na kuchukua hatua za kivitendo za kukabiliana nalo. Aidha taarifa hiyo imetaka nchi za Kiislamu duniani zichukue hatua za kuipokonya Saudia haki ya kusimamia Hija na maeneo matakatifu ya Kiislamu.

Wizara ya Hija na Umra ya Saudi Arabia imetangaza kuwa, ibada ya Hija mwaka huu itafanyika kwa kushirikisha raia  wa ufalme huo na wageni wanaoishi nchini humo wasiozidi elfu 60.

Wakati huo huo Jumuiya ya Maulamaa wa Yemen imelaani uamuzi uliochukuliwa na Saudi Arabia wa kuzuia ibada ya Hijja na Umra kwa Waislamu kutoka nje ya nchi hiyo kwa mwaka wa pili mfululizo.

Taarifa iliyotolewa leo na jumuiya hiyo imesema kuwa, uamuzi wa serikali ya Riyadh wa kuzuia ibada ya Hija kwa mwaka wa pili mfululizo kwa kutumia kisingizio cha maambukizi ya virusi vya corona umechukuliwa kwa shabaha ya kuihudumia Marekani na Israel. 

Taarifa ya Jumuiya ya Wanazuoni wa Kiislamu nchini Yemen imesema uamuzi huo wa kuzuia ibada ya Hija mwaka huu unaenda sambamba na malengo ya Marekini na Israel na si ajabu kwamba umebuniwa na kupikwa Washington na Tel Aviv.

Jumuiya hiyo imesema kuwa, uamuzi wa Wizara ya Hija na Umra ya Saudia wa kuwazuia Waislamu kutoka nje kwenda nchini humo kutekeleza ibada ya Hija kwa mwaka wa pili mfululizo ni wa kidhalimu na kuongeza kuwa, serikali ya Riyadh imechukua uamuzi huo kwa kiburi kikubwa. 

3977254

Kishikizo: yemen hija saudia
captcha