Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo Jumanne katika jibu lake kwa barua ya Meja Jenerali Qassem Suleimani Kamanda wa Kikosi cha Quds katika Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kueleza : "Ninamshukuru Mwenyezi Mungu Mkubwa ambaye amezipa baraka juhudi zako za kujitolea kijihadi pamoja na wenzako katika nyuga mbalimbali na hivyo kupelekea kung'olewa kwa mikono yenu nyinyi waja wema huko Syria na Iraq mizizi ya mti khabithi wa ISIS ambao mche wake ulipandwa na mataghuti wa dunia."
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, hili sio pigo kwa kundi ovu na dhalimu la ISIS pekee, bali hatua hiyo ya kung'olewa mizizi ya ISIS imetoa pigo kubwa pia kwa siasa za kikhabithi za kuanzisha vita vya ndani katika Mashariki ya Kati na kuutokomeza muqawama ulio dhidi ya Israel sambamba na kuyadhoofisha madola na tawala huru kupitia viongozi waovu wa kundi hilo lililopotoka.
Katika sehemu nyingine ya jibu lake kwa barua hiyo, Ayatullah Khamenei amemhutubu Meja Jenerali Qassem Suleimani kwa kumwambia: "Kwa hatua yako na wenzako ya kulisambaratisha donda hili angamizi la saratani, mumezihudumia pakubwa si nchi za Mashariki ya Kati na Ulimwengu wa Kiislamu pekee, bali mataifa yote na jamii nzima ya mwanadamu.
Kadhalika Ayatullah Khamenei ametoa mkono wa kheri na pongezi kwa ushindi huo na kubainisha kwamba, haipasi kughafilika na hila na ghiliba za adui."
Mapema jana Kamanda wa Kikosi cha Quds katika Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, IRGC, alimtumia ujumbe Ayatullah Sayyed Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akitangaza kuangamizwa satwa khabithi ya kundi la kigaidi la ISIS au Daesh.
Kwa mujibu wa tovuti ya Sepahnews, Meja Jenerali Qassem Suleimani Kamanda wa Kikosi cha Quds katika Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu leo Jumanne asubuhi amemtumia ujumbe Ayatullah Khamenei na kutangaza kuwa: "Mimi kama mtumishi na askari mwenye kutekeleza wadhifa kwa niaba yako katika medani hii, ninatangaza hapa kuwa, kufuatia kukombolewa mji wa Al Bukamal, ngome ya mwisho ya ISIS na bendera ya kundi hili la Kimarekani-Kizayuni imeshushwa na mahala pake kupeperushwa bendera ya Syria na kwa msingi huo satwa khabaithi na iliyolaaniwa ya ISIS imefika ukingoni."