IQNA

Makala

Muhtasari wa tukio muhimu la Ghadir katika Uislamu

9:45 - July 07, 2023
Habari ID: 3477248
Leo Ijumaa mwaka 1444 Hijria Qamaria sawa na 7 Julai 2023 inasadifiana na siku kuu ya Ghadir Khum ambayo ni idi kubwa ya Waislamu.

Baada ya Mtume Mtukufu (SAW) kumaliza Hija yake ya mwisho, aliamua kurejea Madina. Akiwa njiani, kulitoa tukio kubwa ambalo lilibadili kabisa historia. Siku hiyo mtukufu huyo aliwataka Waislamu waliokuwa wamekamilisha ibada ya Hija na kuanza kutawanyika wakielekea makwao wakusanyike katika sehemu moja iliyojulikana kwa jina la Ghadir Khum ili apate kuwapa habari muhimu na ujumbe mkubwa kutoka kwa Mola wake. Je kulikuwa na jambo gani ambalo lilikuwa limetokea katika siku hiyo?

Kwa amri ya Mwenyezi Mungu, katika siku hiyo ya Ghadir Mtume (SAW) alimtangaza Imam Ali bin Abi Twalib (AS) kwamba ameteuliwa na Mwenyezi Mungu kuwa kiongozi na khalifa wa Mtume ambaye atachukua nafasi ya mtukufu huyo baada ya kuondoka dunia kuuongoza Umma wa Kiislamu. Tunatoa mkono wa pongezi na fanaka kwa Waislamu wote duniani na hasa wapenda haki na uadilifu, kwa mnasaba wa kuwadia siku hii adhimu.

Mlinzi wa jamii ya Kiislamu

Mtume Mtukufu ambaye alikuwa katika siku za mwisho za umri wake alikuwa na haja ya kuuacha mti mchanga wa Kiislamu katika mikono ya mtu anayeaminika zaidi ambaye angeweza kuulea mti huo kwa njia inayofaa baada ya kuondoka yeye. Katika kipindi cha miaka yote aliyokuwa Mtume, mjumbe huyo wa Mwenyezi Mungu hakuwahi hata siku moja kuiacha jamii ya Kiislamu bila ya mlinzi na mchungaji.

Kila mara alipoondoka katika mji wa Madina, ambayo ndiyo yaliyokuwa makao makuu ya serikali ya Kiislamu katika zama zake, Mtume SAW alikuwa akimchagua mtu wa kusimamia mambo ya Waislamu. Kwa kuzingatia hali ya wasiwasi iliyokuwepo juu ya mustakbali wa Umma wa Kiislamu, jamii ilihitajia viongozi wanaofaa na wa kuaminika ili kufasiri na kutekeleza kwa njia sahihi aya za Qur'ani Tukufu na mafundisho ya Mtukufu Mtume. Ahlul Bait wa Mtume (SAW) wakiongozwa na Imam Ali bin Abi Twalib (AS) ndio waliokuwa chaguo bora zaidi la kutegemewa katika kuwaongoza Waislamu kwa msingi wa Kitabu kitakatifu cha Qur'ani.

Ahlul Bait wa Mtume SAW na Qur'ani Takatifu

Katika siku ya Ghadir Khum iliyosadifiana na tarehe 18 Mfunguo tatu Dhulhijja, Mtume alisisitizia ukweli huo na kutilia mkazo kwamba, Ahlul Bait wake na Qur'ani Takatifu ni vitu viwili vyenye thamani kubwa ambavyo kamwe havitatengana, kwa sababu vitu viwili hivyo ni chimbuko la elimu na siri za hekima ya mbinguni. Hilo ni jambo ambalo lilisisitizwa bayana na Mtume katika siku ya Ghadir.

Tarehe 18 Mfunguo Tatu Dhulhijja mwaka wa 10 Hijiria, msafara wa Mtume na Waislamu ambao walikuwa wamekamilisha ibada ya Hija ulikuwa njiani kurejea Madina na ilikuwa ni karibu na adhuhuri, msafara huo ulipofika eneo liitwalo Ghadir Khum. Mtume wa Mwenyezi Mungu aliwataka Waislamu kusimama katika eneo hilo na akaamuru Waislamu wote waliotawanyika wakusanyike tena ili apate kuwasilisha ujumbe muhimu kutoka mbinguni. Mtume aliwaamuru masabaha wake wanne wa karibu ambao ni Miqdad, Salman, Ammar na Abu Dhar kutengeneza mimbari chini ya mti mmoja mkubwa.

Watu walikuwa wakijiuliza kuhusu umuhimu wa jambo alilokuwa nalo Mtume ambalo lilimlazimimisha awasimamishe katika jangwa hilo pana na lililokuwa na joto kali. Taratibu sauti zilianza kufifia na kimya kikaenea kila upande.

Ujumbe muhimu

Rabia ambaye alikuwa na sauti kubwa alichaguliwa kukariri maneno ya Mtume kwa watu ambao kidogo walikuwa mbali na mtukufu huyo na ambao hawakuweza kusikia vizuri maneneo yake. Baada ya kuswalisha Swala ya Adhuhuri, Mtume alipanda juu ya mimbari ambayo alikuwa ametengenezewa kutokana na vifaa vya ngamia huku akiwa ni mwenye tabasamu na aliyejaa furaha. Kisha alimwita Ali bin Abi Twalib na kumwambia asimame upande wake wa kulia. Mtume ambaye alikuwa ameuweka mkono wake wa kulia katika bega la Imam Ali (AS) alishukuru na kumhimidi Mwenyezi Mungu, na kuwaambia Waislamu waliokuwa wamekusanyika sehemu hiyo kwamba alikuwa na ujumbe muhimu kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambao ameamriwa awafikishie.

Aliwaambia kwamba, lau kama hatoefikisha ujumbe huo ingelikuwa ni kama vile hakutekeleza kabisa jukumu lake alilopewa na Mwenyezi Mungu. Baada ya kuzungumzia mambo kadhaa, Mtume aliunyanyua juu mkono wa Imam Ali bin Abi Twalib (AS) na kusema: "Kila mtu ambaye mimi ni kiongozi wake basi huyu Ali pia ni kiongozi wake. Mwenyezi Mungu ampende atakayempenda Ali, na amfanyie uadui atakayemfanyia uadui." Mtume SAW pia aliwausia Waislamu kushikamana na Qur'ani na Ahlubaiti wake na akasema viwili hivyo havitatengana hadi vitakapomkuta yeye katika hodhi ya Kauthar, Siku ya Kiyama.

"Leo nimekukamilishieni dini yenu"

Baada ya maneno hayo ya Mtume, malaika wa wahyi aliteremka kwa Mtume na kumsomea aya ya 3 ya Suratul Maidah ambayo inasema: "Leo nimekukamilishieni dini yenu, na kukutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni Uislamu uwe dini yenu." Naam, hivyo ndivyo historia ya Ghadir ilivyoanza kusajiliwa na kuainisha mustakbali wa jamii ya mwanadamu.

Ibn Talha Shafi' anasema katika kitabu cha Matalibus Suul kwamba: "Kila maana itakayotolewa kwa neno 'maula' ambalo lilitumiwa na Mtume katika kumuarifisha Imam Ali bin Abi Twalib katika eneo hilo la Ghadiri Khum, litakuwa bila shaka linamhusu Ali, jambo ambalo linatosha kubainisha nafasi ya juu aliyopewa na Mtume (SAW). Kwa msingi huo, siku hiyo ni siku ya furaha," mwisho wa kunukuu.

Sifa za kipekee za Imam Ali

Dakta Iswam al-Imad, mtafiti mashuhuri ambaye mwanzoni alikuwa akifundisha katika vyuo vikuu vya Saudi Arabia, miaka kadhaa iliyopita alisema, amefanya uchunguzi wa kina na kugundua sifa nyingi za Imam Ali (AS) zilizoashiriwa na Mtume Mtukufu (SAW). Anasema: "Katika hadithi za Mtume, baada ya kuashiria suala la Tauhidi, Utume na Siku ya Kiama, nimetambua kwamba mtukufu huyo amemsifu sana Imam Ali (AS). Mtume alikuwa akisisitiza na kujaribu sana kutangaza jina na Imam Ali katika nyakati na sehemu mbali mbali. Sisitizo hilo la Mtume lililokuwa na lengo la kuweka wazi sifa za kipekee za Imam Ali, lilinishangaza na kunistaajabisha mno. Hatimaye baada ya kufanya uchunguzi na utafiti wa muda mrefu nilitambua chanzo na sababu ya mapenzi makubwa ya Mtume kwa Imam Ali bin Abi Twalib (AS). Katika uchunguzi wangu, kwanza nilitambua dhulma kubwa aliyofanyiwa Imam Ali na kuhisi katika nafsi yangu kwamba nilikuwa nimevutiwa sana na mtukufu huyo."

Uchunguzi wa wasomi wa Kiislamu

Tukio muhimu la Ghadir Khum limechunguzwa na kuzungumziwa na wasomi wengi wa madhehebu mbalimbali za Kiislamu. Abul Faraj bin Jauzi Hambali, mmoja wa wanafikra na wasomi wa Kiislamu wa madhehebu ya Kisuni ya Imam Hambali anasema kuhusiana na suala hilo kwamba: "Wataalamu wa historia na sira ya Mtume, wote wanaafikiana kwamba, tukio la Ghadir lilitokea wakati Mtume (SAW) alipokuwa njiani kurejea Madina katika Hija yake ya mwisho. Katika siku hiyo masahaba, Waarabu na wakazi wa viunga vya mji wa Makka wapatao laki moja na elfu 20 walikuwa na Mtume. Hiyo ndiyo idadi ya watu walilosikia hadithi inayohusiana na uongozi wa Ali (AS) kutoka kwa Mtume katika siku ya Ghadir."

Watu wema na wasafi

Tunapasa kuzingatia kuwa, tukio la Ghadir ni la kihistoria linalobeba ujumbe kwamba, ni watu wema na wasafi tu ndio wanaofaa kupewa fursa ya kushika hatamu za kuwaongoza wanadamu. Kama tulivyosema, Tukio la Ghadir ni tukio mashuhuri mno, na hakuna mtu yeyote awezaye kukadhibisha kujiri kwa tukio hilo muhimu la kihistoria.

Sayyid Murtadha Alamal Huda, mwanazuoni mkubwa wa Ulimwengu wa Kiislamu ameandika kuhusiana na suala hili kwamba: "Mtu atakayetaka ushahidi wa ukweli wa habari hii ni sawa na mtu anayetaka ushahidi wa ukweli wa habari ya vita na matukio maarufu yaliyotokea katika maisha ya Mtume wa Mwenyezi Mungu; na ni sawa na kusema kwamba anatilia shaka tukio lenyewe la Hijjatul-wida'a, kwa sababu yote hayo mawili yana umashuhuri wa kiwango kimoja".

Maulamaa wakubwa wa Kisunni, nao pia wameinakili hadithi ya tukio la Ghadir Khum kwa sanadi na mapokezi tofauti. Kwa kutoa mfano, Imam Ahmad bin Hanbal, mmoja wa maimamu wa madhehebu nne za Kisuni amemnukuu katika kitabu chake kiitwacho Al Musnad mmoja wa masahaba wa Mtume aitwaye Zaid bin Arqam akisema: "Tulikuwa tumekusanyika pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu katika bonde liitwalo bonde la Khum, kisha akatoa amri ya kusali. Hapo tukasali Sala ya Adhuhuri pamoja na mtukufu huyo, kisha akasoma khutba; na katika hali ambayo kitambaa kilikuwa kimetundikwa juu ya mti ili aweze kuwa kivulini na kutopigwa sana na mwanga wa joto la jua lenye kuunguza, Bwana Mtume alisema: Je hamjui? Je hamshuhudii kuwa mimi ni bora zaidi kwa kila muumini kuliko nafsi yake mwenyewe? Wote wakasema: Ndiyo! Bwana Mtume akasema: Kila yule ambaye mimi ninamtawalia mambo yake, huyu Ali anamtawalia mambo yake, Ewe Mola mpende kila mwenye kumpenda na mfanye adui kila mwenye kumfanyia uadui".

Sahih Bukhari na Muslim

Hakim Naishaburi, naye pia amenukuu kutoka kwenye vitabu viwili vya maulamaa wakubwa wa Kisuni Bukhari na Muslim ya kwamba:"Wakati Mtume wa Allah alipokuwa anarejea kutoka kwenye Hijjatul-Wida'a alisimama Ghadir Khum na kutoa amri watu wakusanyike chini ya miti. Kisha akasema: Karibuni hivi Mola wangu ataniita na mimi nitaitika wito. Nimekuachieni vitu viwili vyenye thamani kubwa ambapo kimoja ni kikubwa zaidi ya kingine: Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu, basi angalieni mtaamiliana navyo vipi baada yangu. Hakika viwili hivi havitengani abadani hadi vitakapoingia kwangu katika hodhi". Kisha akasema, Mwenyezi Mungu Azza wa Jalla ni mwenye kunitawalia mimi mambo yangu, na mimi ni mwenye kumtawalia kila muumini mambo yake. Kisha akaushika mkono wa Ali na kusema: Kila ninayemtawalia mambo yake, basi huyu Ali anamtawalia mambo yake. Ewe Mola! Mpende atakayeikubali Wilaya yake na mfanye adui kila atakayemfanyia uadui".

Maulamaa wengine wengi wa Kisuni kama Tirmidhi, Ibnu Majah, Ibn Asaakir, Ibn Naiim, Ibn Athir, Khorazmi, Suyuti, Ibn Hajar, Haithami, Ghazali pamoja na Bukhari wamelitaja tukio la Ghadir katika vitabu vyao. Abu Sa'ad Mas'uud bin Nasir Sajistani, mmoja wa maulamaa wa Kisuni ameeleza katika kitabu chake kiitwacho Ad Dirayah fii Hadithil Wilayah kuwa ameinukuu hadithi hii kutoka kwa masahaba 120 wa Bwana Mtume.

Hadithi ya Ghadir ni madhubuti

Kwa hivyo sanadi ya hadithi ya Ghadir ni madhubuti na ya yakini kwa kiasi ambacho hakuna mtu anayeweza kuikana na kuficha uhakika wake. Abdulfatah Abdul Maqsud, mwandishi na mhakiki wa Kimisri ameeleza haya katika kitabu chake alichoandika kuhusu Imam Ali (AS):" Hadithi ya Ghadir, bila ya shaka yoyote ni hakika isiyoweza kubatilishwa, inga'rayo na kuangaza mithili ya mwanga wa mchana".

wapenzi wasikilizaji, moja ya malengo ya hatua hiyo ya kutangazwa Imam Ali AS kuwa kiongozi wa Waislamu na wasii wa Bwana Mtume Muhammad SAW inaonyesha ni aina gani ya jamii ya Kiislamu inayotakiwa kuwa na uongozi wa waja wema zaidi. Kuna uhakika mwingi umejikita ndani ya tukio la Ghadir. Kwa kweli kweli wa tukio hilo ni kwamba kazi iliyofanywa na Bwana Mtume Muhammad SAW kwa ajili ya jamii changa ya Kiislamu ya wakati huo ambayo iliundika katika kipindi cha miaka kumi hivi tangu ulipopata ushindi Uislamu, ilikuwa ni kutatua suala la serikali, uongozi na Uimamu kwa maana yake pana na ndio maana katika tukio la Ghadir Khum baada ya kutekeleza ibada yake ya mwisho ya Hijja na wakati alipokuwa anarejea Madina, aliwatangazia Waislamu mtu wa kushika nafasi yake, naye ni Amirul Muminin Ali bin Abi Talib AS.

Hata hii dhahiri ya tukio hilo pekee ambayo tab'an ni muhimu sana, pia ina mazingatio makubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya watu ambao wanayafanyia utafiti na kuyafuatilia masuala ya jamii ya kimapinduzi. Lakini pia kuna uhakika mwingine mkubwa umejificha ndani ya tukio hilo ambapo kama uma na jamii ya Kiislamu itaziangalia kwa kina nukta za uhakika huo, basi itafanikiwa kupata njia bora na ya wazi ya maisha. Kimsingi ni kwamba kama tukio la Ghadir litachukuliwa na Waislamu wote - wawe Waislamu wa Kishia ambao wanalijua vyema tukio hilo katika upande wake wa uongozi, uimamu na Wilaya, au Waislamu wengine ambao pamoja na kwamba wanakubali kuwa tukio hilo lililotokea lakini hawaliangalii kwa sura ya uongozi, uimamu na Wilaya - kama wote hao leo hii watazitilia maanani na kuzizingatia sana zile nukta muhimu zilizojikita katika tukio la Ghadir, basi wataweza kuwaletea mafanikio mengi Waislamu wote duniani. Miongoni mwa nukta hizo ni kwamba mosi huko kuteuliwa tu mtu mtukufu kama Imam Ali kuwa kiongozi wa Waislamu, pekee kuliweka wazi vigezo anavyopaswa kuwa navyo kiongozi wa Kiislamu.

Kishikizo: ghadir khum
captcha