IQNA

Maulamaa wa Kiislamu walaani takwa haramu la Ufaransa kwa misikiti

16:09 - March 28, 2021
Habari ID: 3473765
TEHRAN (IQNA) - Jumuiya ya Kimataifa ya Wanazuoni wa Kiislamu imelaani wito wa serikali ya Ufaransa iliyowataka maimamu wa misikiti nchini humo kubariki na kuhalalisha ndoa baina ya mashoga na watu wenye jinsia moja, ikisisitiza kuwa wito huo unaonyesha msimamo wa kindumakuwili dhidi ya Uislamu.

Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Dkt. Ali Mohyiddeen Al-Qaradaghi amemtumia barua Waziri wa Uraia wa Ufaransa, Marlène Schiappa akikosoa wito wake unaowataka maimamu wa misikiti nchini humo kubariki na kutetea ndoa baina ya mashoga na watu wenye jinsia moja.

Tarehe 23 mwezi huu wa Machi Waziri Marlène Schiappa alisema katika runinga ya Ufaransa kwamba, "katika hotuba zao, maimamu wa misikiti ya nchi hiyo wanalazimika kukubali haki ya kuoana na kufunga ndoa baina ya mabaradhuli na mashoga."

Akijibu wito huo, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Maulama wa Kiislamu amesema kuwa maamuzi hayo ni ya kichochezi na hayaimarishi anga ya kuishi pamoja kwa amani nchini Ufaransa. Amesema dunia imekuwa kama kijiji kimoja na kwamba maamuzi hasi yanayochukuliwa katika sehemu moja huwa na taathira mbaya katika maeneo mengine ya kijiji hicho. Amesema suala la kuheshimu matukufu ya jamii yenye wafuasi wenye dini tofauti ni sifa ya watu wenye busara na wanasiasa wanaotaka kujenga nchi yenye jamii huru.

Pr. Mohyiddeen Al-Qaradaghi amesema Waziri wa Uraia wa Ufaransa amekiuka hata sheria za Ufaransa kwenyewe na kusisitiza kuwa, uharamu wa ndoa baina ya mashoga na mabaradhuli si makhsusi kwa dini ya Uislamu, bali suala hilo limepigwa marufuku na dini zote za mbinguni.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Wanazuoni wa Kiislamu amesema kuwa maingiliano ya kujamiiana baina ya watu wenye jinsia moja ni vita dhidi ya maumbile ya mwanadamu na taasisi ya familia na amewataka Waislamu wa Ufaransa kutumia vyombo vya sheria kwa ajili ya kupambana na jambo lolote linalobana haki zao za kibinadamu zikitanguliwa na haki na uhuru wa kufuata na kutekeleza mafundisho ya dini.   

3474310

Kishikizo: ufaransa waislamu IUMS
captcha