IQNA

Watetezi wa Palestina

Maelezo kuhusu ukandamizaji wa wanafunzi watetezi wa Palestina nchini Marekani

7:56 - April 28, 2024
Habari ID: 3478745
IQNA-Marekani ndiyo muungaji mkono mkubwa zaidi wa utawala wa Kizayuni wa Israel ambapo serikali ya Biden imetoa msaada mkubwa zaidi wa kijeshi na silaha kwa Tel Aviv wakati wa vita vya Gaza, ambavyo vimeingia katika mwezi wake wa saba.

Hali kadhalika Marekani ni muungaji mkono mkuu wa kisiasa wa Israel katika uga wa kimataifa ambapo imetumia mara kadhaa kura ya turufu katika baraza la Usalama kutetea utawala huo katili unaotekeleza mauaji ya kimbari huko Gaza. Lakini pamoja na uungaji mkono huo, kote Marekani, hasa katika vyuo vikuu kumeshuhudiwa ongezeko la upinzani mkali dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel unaotenda jinai.

Katika maandamano ya hivi karibuni ya kupinga uungaji mkono wa Washington kwa utawala wa Kizayuni kwa njia ya kuidhinisha msaada wa dola bilioni 26 za Marekani kwa utawala huo katika Baraza la Wawakilishi la Marekani na Baraza la Seneti la Marekani, baadhi ya wapinzani wa misaada kwa Israel wamefanya maandamano mbele ya makazi ya kiongozi wa Wademokrat katika Baraza la Wawakilishi la Marekani. Maandamano hayo ya amani yamegeuka kuwa ya vurugu na ghasia baada ya polisi kujaribu kuwatawanya waandamanaji. Katika vurumai hizo polisi waliwakamata waandamanaji wengi wanaopinga utawala wa kibaguzi wa Israel.

Hivi sasa zimepita zaidi ya siku  200 tangu kuanza vita vya Gaza na jinai zisizo na kikomo za utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wasio na hatia wa Palestina kwa uungaji mkono wa kifedha, kijeshi na kisiasa wa serikali ya Biden. Kutokana na jinai hizo za Israell, vyuo vikuu vya Marekani vimekuwa uwanja wa ukandamizaji wa wanafunzi wanaoandamana. Katika kipindi cha miezi saba iliyopita, maandamano makubwa yamefanyika katika vyuo vikuu vya Marekani kupinga uhalifu wa Israel huko Gaza, hasa mauaji ya kimbari pamoja na kutumiwa vibaya njaa kama silaha ya kivita. Aidha wanafunzi hao wanataka hatua za haraka zichukuliwe kuushinikiza utawala katili wa Israel usitishe vita mara moja Gaza. Serikali ya Biden imekasirishwa sana na maandamano hayo ambayo yanafichua jinai za Israel na kwa msingi huo imechukua hatua za kuwakandamiza wanafunzi na wahadhiri wanaoshiriki katika mijumuiko dhidi ya Israel.

 

Taarifa zinasema wanafunzi na wahadhiri wa vyuo vikuu zaidi ya 20 nchini Marekani wanaadanamana takribani kila siku kupinga vita hivyo. Wanafunzi hao wanatoa wito kwa vyuo vikuu kujitenga na makampuni yoyote ambayo yanaendeleza vita vya utawala unaokalia dhidi ya Gaza. Polisi wamewakamata mamia ya waandamanaji katika kampasi za vyuo vikuu.

Ni jambo la kushangaza kwamba wanasiasa wa vyama vikuu vya Demokrat na Republican  wanapinga maandamano ya wanafunzi dhidi ya jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel.

.

Katika muktadha huo, Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump amewaambia waandishi wa habari alipokuwa akienda mahakamani kwa siku ya sita ya kesi yake huko Manhattan alidai kuwa maandamano ya wanachuo wa Marekani dhidi ya Israel ni aibu.

Katika ngazi ya jamii ya Marekani, mielekeo ya kuukosoa utawala wa Kizayuni na kuwaunga mkono Wapalestina imezidi kushika kasi. Matokeo ya uchunguzi wa maoni ya Wall Street Journal, uliofanyika kuanzia tarehe 21 hadi 28 Februari, yanaonyesha kuwa wananchi wengi wa Marekani hawaridhishwi na utendaji wa Joe Biden katika vita vya Gaza na wanaamini kuwa utawala wa Kizayuni umetumia nguvu kupita kiasi kujibu operesheni ya Kimbunga cha Al Aqsa iliyotoekelezwa mnamo Oktoba 7.

Aidha katika uchunguzi mwingine wa nchi nzima uliofanyika mwishoni mwa Januari 2024 nchini Marekani, ilibainika kuwa nusu ya Wamarekani wanaamini kuwa utawala wa Kizayuni unafanya mauaji ya kimbari huko Gaza dhidi ya Wapalestina.

Uvamizi wa Israel dhidi ya Gaza hadi sasa umeua zaidi ya watu 34,000 wengi wao wakiwa wanawake na watoto na kuwaacha  wengine zaidi ya 77,000 wakiwa wamejeruhiwa. Idadi kubwa ya wakazi milioni 2.3 wa Gaza wameyakimbia makazi yao huku makundi ya kutetea haki za binadamu yakisema hakuna sehemu salama huko Gaza.

3488099

 

Habari zinazohusiana
captcha