IQNA

Fatwa ya IUMS: Uungaji Mkono Palestina ni Jukumu la Kiislamu

17:19 - May 18, 2021
Habari ID: 3473922
TEHRAN (IQNA)- Jumuiya ya Kimataifa ya Maulamaa Waislamu (IUMS) imetoa Fatwa inayobainisha kuwa, kuunga mkono Palestina ni jukumu la Kiislamu.

Katika taarifa, IUMS imetoa wito kwa Waislamu wote kuwasaidia Wapalestina ambao wanakabiliwa na hujuma ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Taarifa hiyo imesema ni jukumu la kila Mwislamu kuunga mkono Palestina na wale wanaoulinda Msikiti wa Al Aqsa kadiri wanavyoweza.

Taarifa hiyo imesema kitendo chochote ambacho kinaupa nguvu utawala wa Kizayuni wa Israel, ikiwa ni pamoja na kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala huo ni Haramu. IUMS imesema uharamu wa hilo unatokana na kuwa kushirikiana na Israel ni sawa na kushiriki katika jinai zake dhidi ya taifa la Palestina.

Halikadhalika IUMS imetoa wito kwa Waislamu kuwaunga mkono Wapalestina na Msikiti wa Al Aqsa kifedha, kisiasa na njia zinginezo.

Kwa mujibu wa takwimu za karibuni zilizochapishwa na Wizara ya Afya ya Palestina, katika duru hii mpya ya mashambulio ya utawala wa kibaguzi wa Israel, Wapalestina wasiopungua 220 wamepoteza maisha wakiwemo watoto 60, na zaidi ya 5600 wengine wamejeruhiwa.

Katika kipindi cha wiki moja iliyopita, Umoja wa Mataifa umefanya vikao mara tatu kwa lengo la kujaribu kusimamisha mashambulizi hayo ya kinyama ya Israel dhidi ya watu wasio na hatia lakini bila mafanikio yoyote na hilo ni kutokana na ukwamishaji wa Marekani ambayo haitaki kuona utawala huo wa Kizayuni ukichukuliwa hatua za kisheria.

Utawala ghasibu wa Israel ulianzisha uvamizi dhidi ya Ghaza baada ya Wapalestina katika eneo hii kuandamana kulalamikia vikali ukandamizaji wa Israel dhidi ya Wapalestina katika mji wa Quds (Jerusalem). Kitendo cha askari katili wa Israel kuuvamia Msikiti wa Al Aqsa mjini Quds na kuwahujumu Wapalestina waliokuwa wakiswali katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kimehesabiwa kuwa ni kuvuka mstari mwekundu wa Wapalestina na Waislamu duniani.

Katika kujibu jinai hizo za Israel makundi ya kupigania ukombozi wa Palestina katika Ukanda wa Ghaza yamevurumisha mamia ya makombora katika miji ya Israel ukiwemo mji wa Tel Aviv na kusababisha hasara kubwa.

3972115

captcha