IQNA

Kikao cha Kimataifa cha Qur'ani na Vijana Waislamu wafanyika Shiraz, Iran

18:23 - October 31, 2017
Habari ID: 3471239
TEHRAN (IQNA)-Kikao cha Qur'ani Tukufu na vijana Waislamu duniani kinafanyika katika mji wa Shiraz kusini mwa Iran.
Kikao cha Kimataifa cha Qur'ani na Vijana Waislamu wafanyika Shiraz, IranKwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, vijana 700 wanaharakati wa Qur'ani kutoka Iran na maeneo mengine duniani wanahudhuria kongamano hilo la siku tatu lililoanza Jumatatu.

Akizungumza wakati wa kufungua kongamano hilo, Heidar Ali Kamyab Kalantari, Mkurugenzi wa Mipango ya Kimataifa katika Mji Mkuu wa Vijana Waislamu katika Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC, mwaka 2017, amesema kushiriki vijana kutoka maeneo mengine ya dunia na hasa uwepo wa Mufti Mkuu wa Uturuki katika kikao hicho ni fursa ya kustawisha utamaduni wa Amani na urafiki. Ufunguzi wa kikao hicho umefanyika katika Haram Takatifu ya Shah Cheragh AS mjini Shiraz.

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC mwaka jana iliutangaza mji wa Shiraz kusini mwa Iran kuwa mji mkuu wa vijana katika Ulimwengu wa Kiislamu mwaka 2017.

Mji wa Shiraz katika mwaka wa 2017 ni mwenyeji wa vijana wa nchi za Kiislamu ambao watashiriki katika shughuli zinazohusu mji huo kama mji mkuu wa vijana wa ulimwengu wa Kiislamu.

Kwa zaidi ya miaka 2,000 mji wa Shiraz umekuwa ukitambuliwa kama kitovu cha utamaduni wa Kiajemi au Kifarsi na ni mashuhuri kama kituo cha elimu, ustaarabu na fasihi.

Aidha Shiraz ulikuwa moja ya miji muhimu zaidi ya ulimwengu wa Kiislamu katika zama za kuanzia karne za 9-13 Miladia. Aidha mji wa Shiraz ulikuwa mji mkuu wa Iran katika zama za utawala wa ufalme wa Zand kuanzia mwaka 1747-79 Miladia na ni katika kipindi hicho ndipo majengo yake maridadi zaidi yalijengwa au kukarabatiwa.

Mjini Shiraz pia kuna kaburi au ziara la Shah Cheragh, mwana wa Imam Musa Kadhim AS ambaye ni kati ya Maimamu watoharifu wa Ahlul Bayt (Watu wa Nyumba) wa Mtume Muhammad SAW.

Halikadhalika mjini Shiraz kuna makaburi ya Hafez na Saadi, malenga wawili mashuhuri zaidi Wairani.


3464303
captcha